Nia za papa

Nia za Sala za Papa kwa Mwaka 2024

Januari

Kwa kipawa cha wingi wa karama mbalimbali Kanisani, tumuombe Roho Mtakatifu atusaidie kutambua zawadi ya karama mbalimbali ndani ya jumuiya za Kikristo na kugundua utajiri wa mapokeo, desturi na taratibu tofauti katika Kanisa Katoliki.

Februari

Kwa wagonjwa walio mahututi, tuwaombee wale wenye magonjwa yaliyokubuhu, pamoja na familia zao, wapokee huduma muhimu zinazohitajika za kimwili na kiroho pamoja, usaidizi na uangalizi.

Machi

Kwa mashahidi wapya, tuwaombee wale wanaoweka maisha yao hatarini kwa ajili ya kusambaza injili katika sehemu mbalimbali za ulimwengu wachochee na kuimarisha Kanisa kwa ujasiri wao na hamasa ya kimisionari.

Aprili

Kwa nafasi ya wanawake, tuombe kwamba hadhi na thamani kuu ya wanawake itambulike katika kila tamaduni, na kutokomeza ubaguzi wanaokutana nao katika sehemu mbalimbali za ulimwengu.

Mei

Kwa malezi ya watawa na waseminari, tuwaombee watawa wanawake na wanaume, pamoja na waseminari, wakue na kuimarika katika miito yao kupitia malezi ya kichungaji, kiroho, ya utu na ya kijamii, yawasaidie kuwa mashahidi imara na wakuaminika katia Injili.

Juni

Kwa wahamiaji wanaokimbia makwao, tuwaombee wahamiaji wanaokimbia vita au njaa, wanaolazimika kufanya safari zilizo jaa hatari na ghasia mbalimbali, wakaribishwe na kupata fursa mpya katika nchi zinazowapokea.

Julai

Kwa huduma ya kichungaji kwa wagonjwa, tuombe kwamba Sakramenti ya mpako wa wagonjwa iwape wale wanaoipokea na wapendwa wao nguvu za Bwana na kuwa ishara inayoonekana ya huruma na ya matumaini kwa wote.

Agosti

Kwa viongozi wa siasa, tuwaombee viongozi wa siasa wawatumikie watu wao, wakifanya kazi kwa ajili ya maendeleo kamilifu ya binadamu na kwa ajili ya manufaa ya wote, hasa kuwatunza maskini na wale waliopoteza kazi zao.

Septemba

Kwa kilio cha dunia, tuombe kwamba kila mmoja wetu asikie na kuguswa moyoni na kilio cha dunia na waathirika wa majanga ya asili na mabadiliko ya hali ya hewa, na kwamba kila moja kwa nafsi yake atajitahidi kuutunza ulimwengu tunaoshi.

Oktoba

Kwa utume shirikishi wa pamoja, tuombee Kanisa liendelee kudumisha mwenendo wa Sinodi katika namna zote, kama ishara ya uwajibikaji wa pamoja, kukuza ushirikishwaji, ushirika na utume wa pamoja kati ya mapadre, watawa na walei.

Novemba

Kwa wale waliopoteza mtoto au watoto, tuwaombee wazazi wote wanaoomboleza kupoteza mtoto au watoto, wapate msaada kutoka kwenye jamii zao na wapokee amani na faraja kutoka kwa Roho Mtakatifu.

DesembaKwa wanahija wa matumaini, tuombe ili Mwaka huu wa Jubilei uimarishe imani yetu, ukitusaidia kumtambua Kristo Mfufuka katika maisha yetu ya kila siku, na utubadilishe tuwe wanahija wa tumaini katika Kristo.